Kufuatia kufungwa kwa benki ya Chase siku ya Alhamisi wakazi kutoka Kaunti ya Mombasa wanataka serikali kupitia kwenye benki kuu ya Kenya kubuni sheria kali dhidi ya wakurugenzi wakuu wa benki ambazo zimepatikana na hatia ya matumizi mabaya ya nafasi yao vibaya.
Wakiongea na mwandishi habari huyu kwenye masoko mawili maarufu ya Markiti na Kongowea, jijini Mombasa, baadhi ya wafanyabiashara hao wameitaka serikali kuanzisha uchunguzi haraka kuhusiana na kufungwa kwa benki hiyo na kuweza kurudisha imani ya wateja pamoja na wawekezaji wa taasisi mbalimbali baina na sekta ya benki nchini.
Sureyha Abdi ambaye ni mteja na mfanyabiashara wa vitambaa na nguo hasa za kina mama wa kiislamu katika soko kuu la Markiti amesema kuwa yeye alikuwa mmoja wa wateja wa benki hiyo lakini alibahatika kuondoa hela zake wiki moja kabla ya kufungwa na kudai kuwa aliona dalili hizo mapema baada ya ripoti za kudorora kwa huduma za benki hiyo mwezi jana.
“Ilinibidi nikaondoa hela zangu wiki iliyopita, baada ya kushauriwa na mume wangu, na pia nilikuwa natarajia kusafiri wiki hii Jumamosi kuenda kuagizia nguo na bidha nyingine za kibiashara, nashukuru, na ningependa benki kuu ya Kenya kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika,” aliongeza mfanyabiashara huyo.
Kwenye soko kuu la Kongowea wito ulikuwa uo huo, ambapo wengi wa wafanyabiashara ambao waliongea wameinyoshea serikali kuu kidole cha lawama kwa kuwaacha washukiwa huru huku wateja wakipoteza imani yao kwenye taasisi hizo.
Wafanyabiashara hao kwa sauti moja kupitia Samson Kioko wametaka wakaguzi wakuu wa serikali maarufu kama ‘Auditors’ kuchunguzwa huku wahisi kuwa huenda wanashirikiana na walaghai kwenye taasisi za kifedha kuficha ukweli wanapofanya ukaguzi wao.