Wafanyibiashara wa soko la Daraja Mbili mjini Kisii wametoa makataa ya wiki mbili lau sivyo waandamane kuishinikiza serikali ya kaunti kukarabati soko lao.
Wafanyibiashara hao wanasema serikali imekuwa ikitoa ahadi za uongo bila kutimiza haswa gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae anapolitembelea huwapa ahadi asizotimiza.
Wakizungumza katika soko hilo la Daraja Mbili wafanyibiashara hao wakiongozwa na Vincent Mokua, Irene Moige na wengine walisema kile watafanya ili semi zao zipate maana ni kuandamana na kutotoa ushuru ili kuilazimisha serikali kujali maslahi yao.
“Siku hizi hatuuzi kitu maana mvua hunyesha kuanzia majira ya saa nne asubuhi, watoza ushuru nao wako ange kutuitisha ushuru bila kudadisi hali ya soko lilivyo,” alikiri Mokua.
“ Tutaandamana ndani ya wiki mbili sijazo kulazimisha serikali ya kaunti kukarabati soko na huenda tusitoe ushuru ikiwa kaunti haitaonyesha dalili ya kukikidhi mahitaji yetu,” alisema Mogire.