Wafanyikazi wa viwanda vya kutengeneza nguo za kuuzwa katika masoko ya nje EPZ huko Changamwe mjini Mombasa wamezidi kulalamikia dhuluma wanazopitia kutoka kwa waajiri wao na wakaitaka Serikali kuu na ile ya Kaunti kuingilia kati ili kukomesha dhuluma hizo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akitoa kauli hiyo katika kiwanda kimoja cha EPZ  huko Jomvu katika eneo la Changamwe siku ya Ijumaa, Kiongozi wa Wafanyikazi wanaodai malimbikizi ya mishahara yao tangu mwezi Januari mwaka huu katika kiwanda hicho Phylister Kanga amesema kwamba Wafanyikazi hao wanapitia dhuluma ya hali ya juu.

Phylister amesema kwamba muajiri wao aliwahadaa kwamba tatizo lilikuwa ni kuzuiliwa kwa fedha katika benki ya ‘Chase’ iliyowekwa chini ya mrasimu, lakini licha ya benki hiyo kufunguliwa mwezi Aprili, Wafanyikazi hao bado hawajalipwa.

"Tunasikitishwa sana na jinsi wasimamizi wa kampuni hii wanavyoendesha shughuli zao kwani tangu mwezi Januari hadi sasa hatujalipwa misharaha yetu tumelalamika hadi tumechoka bado hatujalipwa",alisema Phylister.

Akiwahutubia zaidi ya Wafanyikazi wa kiwanda hicho 250 waliyokongamana nje ya kiwanda hicho huko Jomvu mjini Mombasa, Mwakilishi wa Wadi ya Jomvu katika bunge la Kaunti ya Mombasa Karisa Nzai ameikosoa Wizara ya Leba kwa utepetevu na akasisitiza kwamba ni lazima Serikali kuu ichunguze uzembe na ufisadi unaoikumba Wizara hiyo.

Mzozo huo kati ya wafanyikazi wa kiwanda cha EPZ cha ‘Long yan’ na muajiri wao unajiri siku moja tu baada ya Viongozi wa Vijana kaunti ya Mombasa kuwataka Maafisa wa Leba katika kaunti hiyo kuwajibikia unyanyasaji wa wafanyikazi inayokumba sekta ya EPZ katika kaunti ya Mombasa.