Huku wakaazi wa kaunti ya Nakuru wakijiunga na ulimwengu wote kwa matayarisho ya siku ya wafanyakazi duniani Jumapili, maswala ya utendakazi na mishahara yanazidi kuwa changamoto kuu humu nchini.
Baadhi ya wanaofanya kazi za nyumbani waliozungumza na mwandishi huyu mjini Nakuru Alhamisi hii wamelalamikia mazingira duni ya kazi pamoja na mishahara midogo.
Aidha, baadhi ya wakaazi wa Nakuru wanasema wamelazimika kuwacha kuajiriwa ili waanzishe biashara kwani mishahara wanayopata haitoshi kukidhi mahitaji yao.
Wengine nao wamelalamika kuhusu juhudi zisizotosha za kudhibiti kuongezeka kwa gharama ya maisha pamoja na ufujaji wa fedha wanazotoa kama kodi.
‘Mishahara ni duni. Mtu analipwa fedha ambazo hawezi hata kukidhi mahitaji yake. Wanaolipwa mishahara duni ni waalimu nikiwa mmoja wao. Hata sasa nimeamua kufungua biashara yangu ili nipate fedha za kujitosheleza,’ alisema Jacinta Wanjiru.
Ni matamshi yanayojiri huku muungano wa waajiri nchini (FKE) ukiitisha kikao na pande husika kuzungumzia tadhmini ya kiwango cha chini cha mishahara kinachozingatiwa na sheria, wakidai kunyanyasika kwa waajiri katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
kwa upande wake, katibu mkuu wa muungano wa wafanyikazi nchini (Cotu) Francis Atwoli ameikashifu hatua hiyo huku akiwataka FKE kuzingatia maslahi ya wafanyikazi wanaopata mishahara ya chini huku akipendekenza mshahara wa mwananchi wa chini zaidi kufikia angalau elfu kumi na tano.