Shughuli za kawaida mjini Mombasa zilikatizwa kwa muda siku ya Alhamisi baada ya wafanyikazi wa Kiwanda cha kutengeneza nguo cha Mombasa Apparel EPZ, kilichoko eneo la Changamwe, kufanya maandamano.
Wafanyikazi hao waliokuwa wamebeba mabango, walimtaka mkuu wa Idara ya Leba katika Kaunti ya Mombasa, John Nyaga, kung’atuka mamlakani kwa madai ya kushirikiana na waajiri wa viwanda hivyo kuwanyanyasa wafanyikazi.
Wakizungumza na wanahabari nje ya afisi za Leba mjini Mombasa wakiongozwa na Athman Sudi, wafanyikazi hao walisema kuwa lazima mkuu huyo wa Idara ya Leba katika Kaunti ya Mombasa John Nyaga, Waziri wa Leba nchini Phyllis Kandie pamoja na mkurungezi mkuu wa kampuni hiyo kujiuzulu kwa kudai kuwa hakuna usaidizi wowote wanatekelezea wafanyikazi.
"Tunamtaka afisa wa Leba Mombasa John Nyaga na Waziri wa Leba nchini kujiuzulu kwa kuwa wameshindwa kuwasaidia wafanyikazi wanyonge, ishara kamili kuwa wanashirikiana na waajiri wa viwanda kuwanyanyasa wafanyikazi," alisema Sudi.
Wafanyikazi hao walisema watatatiza shughuli za kiwanda hicho iwapo matakwa yao hayatashughulikiwa kwa wakati ufaao.
Walisema kuwa waliachishwa kazi mwanzoni mwa mwaka huu bila ya idhani, na kudai kuwa serikali imewatenga.