Share news tips with us here at Hivisasa

Siku chache tu baada ya kusimamishwa kazi kwa maafisa wa ngazi za juu wa shirika la bandari nchini KPA, kamati kuu inayosimamia bandari hiyo imetangaza kuanza kuchunguza vyeti vya masomo vya wafanyikazi wa shirika hilo.

Hatua hiyo inanuia kuimarisha utendakazi wa shirika hilo kwa kutimuliwa kwa watakaopatikana na vyeti ghushi.

Akiongea na waandishi wa habari siku ya Jumamosi, kwenye makao makuu ya shirika hilo jijini Mombasa, mwenyekiti wa bodi kuu ya bandari nchini Marsden Madoka, alisema kuwa hatua hiyo ni mojawapo ya mikakati ya kuhakikisha kuwa shirika hilo linarejelea hadhi yake ya zamani.

Madoka alisisitiza kuwa sharti kila mfanyikazi wa shirika hilo ajiweke tayari kufanyiwa utathmini na ukaguzi wa vyeti vyake rasmi vya masomo.

Aidha, Madoka alisema kuwa kwa ushrikiano na maafisa wakuu walioteuliwa, watafanya kila juhudi kubadilisha sura ya shirika hilo.

Alisema kuwa vituo vya kuweka shehena vya kibinafsi vitasitishwa kwa sasa ili kuwawezesha kushughulikia masuala mengine ambayo yameleta mtazamo hasi miongoni mwa wawekezaji pamoja na umma kwa jumla.

Mwenyekiti huyo alikuwa ameandamana na kaimu mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Catherine Mturi Wairi, ambaye alichukua hatamu baada ya kusimamishwa kwa aliyekuwa mkurugenzi mkuu Gichiri Ndua.

Hatua hiyo imetajwa na wengi hasa wenyeji katika eneo la Pwani kama itakayohakikisha kuwa ufisadi unakabiliwa.