Wafuasi wa mrengo wa Cord jijini Mombasa wamepinga utafiti uliofanywa na shirika la Infotrack, unaonyesha Rais Uhuru Kenyatta anaongoza kwa umaarufu kwa asilimia 45, huku kinara wa Cord Raila Odinga akifuata kwa asilimia 28, naye Kalonzo Musyoka akifuata kwa asilimia 2.5.
Kwenye mahojiano ya kipekee na mwanahabari huyu siku ya Jumatatu, wafuasi hao walisema kuwa utafiti huo si wa ukweli na kuutaja kama wa kuwadanganya Wakenya.
Wakiongozwa na Hassan Salim, wakaazi hao wa eneo la Mwembe Tayari, walidai kuwa shirika la Infotrack linaendeshwa kwa misingi ya kisiasa wala halina ukweli wowote.
Utafiti huo ulionyesha kuwa mrengo wa Jubilee ni maarufu kwa asilimia 40.4 huku Cord ikiwa na asilimia 31.
Aidha, ulionyesha kuwa Mrengo wa Jubilee ni maarufu katika eneo la North Eastern, Central, Rift Valley na Nairobi, huku Cord ikiwa maarufu katika eneo la Pwani, Magharibi ya Kenya na Nyanza, na eneo la Mashariki mwa Kenya likiwa na umarufu sawa kwa mirengo yote miwili.
Wakati huo huo, Wakenya wameonyesha kutokuwa na imani na Tume za EACC, IEBC na idara ya mahakama nchini.
Asilimia 70 ya Wakenya hawana imani na EACC huku asilimia 50 wakiwa hawana imani na IEBC.
Hata hivyo, utafiti huo ulionyesha kuwa Wakenya wako na imani kubwa kwa vyombo vya habari nchini.
Watu 1, 800 walihojiwa katika utafiti huo kote nchini kati ya Machi 6, 2016 na 10, 2016.