Wafuasi wa Cord jijini Mombasa wamekashifu hatua ya kurushiwa vitoa machozi kwa viongozi wa mrengo wa Cord pamoja na wafuasi wao.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakiongozwa na Olum Odour, wakaazi hao walisema kuwa kitendo hicho ni cha kuvunja moyo ikizingatiwa kuwa maandamano ni haki ya raia kikatiba.

Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatatu, wakaazi hao walikitaja kitendo hicho kama chenye msukumo wa kisiasa na kuhujumu haki za Mkenya.

Kauli hii inajiri baada ya polisi kuwarushia vitoa machozi viongozi wa Cord na wafuasi wao walipojaribu kuingia katika afisi za Tume Huru ya Uchauguzi na Mipaka IEBC, katika jumba la Anniversary Towers jijini Nairobi.

Maandamano hayo yaliyoongozwa na vinara wa Cord Raila Odinga, Moses Wetangula na Kalonzo Musyoka yalilenga kutambulisha serikali kuwa tume ya IEBC haiwezi kusimamia uchaguzi ujao kwa kukumbwa na makosa mengi ya kimaadili.

Viongozi hao wameahidi kurudi tena katika afisi hizo hadi watakapopata nafasi ya kutoa malalamishi yao.