Mwakilishi wa eneo la uwakilishi wadi ya Nyamaiya Laban Masira ambaye pia ni kiongozi wa walio wengi kwenye bunge la kaunti ya Nyamira amewataka wafuasi wa mrengo wa Cord kutoshiriki uchaguzi mkuu ujao iwapo tume ya IEBC itakuwa ingali afisini.
Akiwahutubia wafuasi wa muungano huo mjini Nyamira wakati wa kushiriki maandamano dhidi ya makamishna wa IEBC, Masira aliwarahi wafuasi hao kuepuka kushiriki uchaguzi mkuu ujao kwa kile alichosema kuwa uchaguzi hautakuwa wa huru na haki iwapo tume hiyo itakuwa ingali ofisini.
"Ni ombi langu kwa wafuasi wa muungano wa Cord kutoshiriki kwenye uchaguzi mkuu ujao iwapo tume ya IEBC itakuwa afisini kwa maana hatuamini utendakazi wa tume hiyo kwa kuwa inaegemea upande mmoja," alisema Masira.
Masira aidha aliongeza kwa kuwarahi wafuasi wa muungano wa Cord kuendelea kushiriki maandamano hadi tume hiyo itakapoondoka afisini.
"Ombi langu kwa wakenya wa matabaka mbalimbali nchini ni kuendelea kujitokeza kwa wingi kila Jumatatu kwa maandamano dhidi ya tume ya IEBC," aliongeza Masira.