Wafuasi wa Jubilee katika Kaunti ya Mombasa wamepinga uzinduzi wa Ruwaza ya 2035 na Gavana wa Mombasa Hassan Joho, kwa kuutaja uzinduzi huo kama njia ya kujipigia debe katika uchaguzi mkuu wa 2017 na mwaka 2022.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wafuasi hao, wakiongozwa na Hussein Salim, walisema kuwa wananchi wanataka kuona maendeleo kwanza kabla ya viongozi kuja kwenye majukwaa na kuanza kujipigia debe pasi kutekeleza maendeleo yoyote.

Wakizungumza siku ya Jumapili huko Jomvu, wafuasi hao walidai kuwa Gavana Joho si kiongozi wa vitendo na maendeleo, bali ni kiongozi wa kujipigia debe na porojo kwenye majukwaa, huku mwananchi mlala hoi akipata shida mashinani.

“Gavana Joho anatumia ruwaza hii kujipigia debe hasa baada ya kutangaza hadharani azma yake ya kutaka kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022,” alisema Salim.

Kauli hii inajiri baada ya Gavana Joho kuzindua ruwaza ya mwaka 2035 siku ya Jumamosi katika uwanja wa Mombasa Golf.

Joho alieleza kuwa ruwaza hiyo itajumuisha mpangilio mpya wa kisasa wa jiji la Mombasa, utakaobadilisha taswira ya jiji hilo katika sekta mbalimbali.

Aidha, aliongeza kuwa wanampango wa kutibu maji ya bahari ili kuanza kutumika majumbani, na kusisitiza kuwa hatua hiyo itapunguza tatizo la maji Pwani.