Wafuasi wa Jubilee wakiongozwa na aliyekuwa mgombea wa kiti cha useneta Kaunti ya Mombasa Hazel Katana wakisherehekea uamuzi wa Mahakama ya Upeo. [Picha/ nation.co.ke]

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wafuasi wa Jubilee wamejitokeza jijini Mombasa kusherehekea baada ya Mahakama ya Upeo kuidhinisha ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta.Wafuasi hao wameandamana katikati mwa jiji la Mombasa huku polisi wakiimarisha usalama katika maeneo ambayo wafuasi hao walikita kambi.Wakihutubia wanahabari siku ya Jumatatu katika bustani ya Mama Ngina jijini Mombasa, wafuasi hao wakiongozwa na Waziri wa Utalii Najib Bala walipongeza mahakama hiyo ya juu pamoja na Jaji mkuu nchini David Maraga kwa uamuzi huo.Balala ameutaka upande wa upinzani kukubali uamuzi huo huku akiwasihi kudumisha amani.“Uamuzi ushatolewa sasa ni wakati wa kudumisha amani kote nchini. Sio lazima kuanza machafuko,” alisema Balala.Balala alisema kuwa Jubilee itazidi kuboresha maisha ya jamii na kuinua uchumi wa taifa kwa jumla.“Jubilee itazidi kuboresha uchumi na maisha ya wanyonge kote nchini bila kujali rangi ama kabila,” alisema Balala.Kwa upande wake, aliyekuwa mgombea wa kiti cha useneta Kaunti ya Mombasa kupitia chama cha Jubilee Hazel Katana amemtaka kinara wa NASA Raila Odinga kuwaonya wafuasi wake dhidi ya kuzua fujo.“Sharti upande wa upinzani uwaonye wafuasi wao dhidi ya kuzua fujo zisizokuwa na manufaa,” alisema Katana.Hata hivyo, Katana aliwasihi Raila na Uhuru kufanya mazungumzo kama njia moja ya kuhakikisha utulivu unarejea nchini.Kwengineko, baadhi ya wafuasi wa chama cha Jubilee kutoka Kaunti ya Kwale wamejitokeza kusherekea uamuzi huo wa Mahakama ya Upeo.Wakiongozwa na aliyekuwa mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Kwale Zainab Chidzuga, wameutaja ushindi wa Uhuru kama ujio wa amani nchini.Aidha, wamewashtumu vikali viongozi wa NASA kwa madai ya kuwachochea vijana kuzua vurugu unaosababisha uharibifu wa mali.