Wafuasi wa Jubilee katika Kaunti ya Mombasa wamepongeza hatua ya kuandolewa mashtaka kwa Naibu Rais William Ruto na mwanahabri Joshua Arap Sang.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakizungumza siku ya Jumanne, wafuasi hao wakiongozwa na Shabal Hammed, walisema kuwa huo ni ushindi mkubwa kwa taifa la Kenya.

Hammed alisema kuwa wanafuraha ikizingatiwa haki imepatikana kwa wawili hao ambao kwa muda walikuwa wanatatizika kutimiza majukumu yao kwa kuhudhuria vikao vya kesi hiyo.

Aidha, waliilaumu Mahakama ya ICC kwa madai ya kutumiwa kisiasa kuhujumu viongozi wa Afrika.

Hatua hii inajiri baada ya Mahakama ya ICC kutoa uamuzi kuwa Naibu Rais William Ruto na mwanahabari Joshua Arap Sang hawana kesi ya kujibu kuhusiana na mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu yaliyokuwa yanawakabili.

Ruto alikabiliwa na mashtaka ya mauaji, kuhamisha watu kwa lazima na mateso yaliyotekelezwa wakati wa vita vya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

Alikana mashtaka hayo na mawakili wake walitaka kesi hiyo itupiliwe mbali kutokana na ukosefu wa ushahidi.

Watu takriban 1,200 waliuawa wakati wa mapigano hayo.

Majaji walisema upande wa mashtaka haukutoa ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai dhidi ya Ruto na Sang.

Disemba mwaka 2014, mwendesha mashtaka aliondoa mashtaka sawa dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta akisema mashahidi walikuwa wametishiwa na kubadilisha ushahidi wao.

Ruto na Kenyatta walikuwa kwenye mirengo pinzani wakati wa uchaguzi wa 2007 lakini waliunda muungano wa kisiasa na wakashinda uchaguzi mkuu wa 2013.