Uamuzi wa bodi ya uchaguzi ya chama cha ODM kuhairisha uchaguzi wa mashinani kwenye maeneo mbalimbali katika Kaunti ya Nyamira haujapokelewa vizuri na baadhi ya maafisa wa chama hicho kutoka Borabu.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakiongozwa na mwenyekiti wa vijana Bw Moseti Bwongeri, wanachama hao wa ODM walilalamikia kutohusishwa kwa wawaniaji wa nyadhifa mbalimbali kwenye maamuzi hayo huku wakipuuza madai ya viongozi wakuu wa chama kuwa kungelishuhudiwa vurugu kwenye chaguzi hizo.

"Tunalalamikia hatua ya viongozi wakuu wa chama kufanya maamuzi ya kuhairisha uchaguzi mashinani hata bila yakuwahusisha wawaniaji wa nyadhifa mbalimbali. Tunapuuza madai ya baadhi ya viongozi kuwa kungelishuhudiwa vurugu wakati wa uchaguzi kwa kuwa hayana msingi," alisema Bwongeri.

Aidha, Bwongeri aliongeza kusema kuwa huenda hatua yakuhairishwa kwa uchaguzi huo ilisababishwa na baadhi ya wawaniaji ambao waliogopa uchaguzi wa siri kwa maana labda hawana hakika yakushinda.

"Sisi kama viongozi wa chama tunaoondoka hatujafurahishwa na uamuzi wa kuhairishwa kwa uchaguzi. Tunataka kupewa maelezo na bodi ya uchaguzi wa chama cha ODM kuhusu na ni kwanini uchaguzi huo ulihairishwa," alisema Bwongeri.

Aliongeza, "Kama wanachama wa ODM hatuwezi kosa kutaja wazi kwamba huenda uchaguzi huu ulihairishwa ili kuwateua moja kwa moja watu wachache wanaopendelewa na chama kushikilia afisi kwa miaka mitatu ijayo. Kamwe hatutalikubali hilo kutendeka."

Haya yanajiri baada ya barua iliyotiwa sahihi na kinara wa chama cha ODM Raila Odinga kusambazwa kwenye afisi za chama hicho katika Kaunti ya Nyamira.

Barua hiyo ilisema kuwa uchaguzi huo utahairishwa kutoka tarehe Octoba 31 hadi Novemba 23, 2015 kwa sababu yakushukiwa kushuhudiwa vurugu kwenye uchaguzi huo.