Idara ya Mifugo katika Kaunti ya Kisii imewaomba wafugaji wote kutoka Kaunti hiyo kutoa ripoti kwenye ofisi zao kuhusu kisa chochote cha maradhi ya mifugo zao.
Kwenye mahojiano ofisini mwake, Afisa anayesimamia maradhi ya mifugo wa nyumbani Daktari George Ondande amesema kuwa wafugaji wote sharti wawasilishe kisa chochote wanachoshuku cha ugongwa kwa wanyama wao ili kuepusha kusambaa kwa magonjwa hayo kwa mifugo wengine.
Daktari Ondande alisisitiza umuhimu wa kuweka rekodi za afya za mifugo kama mbinu mojawapo ya kurahisisha shughuli wakati wa kupeanwa dawa kwa mnyama ambaye ameathiriwa.
Daktari huyo alionya kuwa iwapo wafugaji hawatawafahamisha Mafisaa wa Idara ya mifugo, huenda kukatokea vifo zaidi kutokana na maradhi haswa nyakati hizi za mvua nyingi katika maeneo ya Kisii.
“Tukiwajibikia mifugo yetu kwa kutoa ripoti za afya na kuulizia ushauri kutoka Idara yetu, bila shaka itawanaufaisha wafugaji wetu na hivyo kuwa hali nzuri ya kupiga hatua kiuchumi,” alishauri Daktari Ondande.
Kisii ni miongoni mwa Kaunti ambazo zimejikita katika ufugaji mseto wa kisasa na Mafisaa wa Kilimo na Madaktari wa mifugo wameonyesha juhudi kubwa kushirikiana na wakulima katika siku za hivi karibuni.