Mkurugenzi Mkuu wa idara ya samaki na viumbe wa maji kwenye Kaunti ya Kisii Edwin Muga amewataka wanaofuga samaki kujiunga na kundi mbali mbali ili kuimarisha bei ya samaki kwenye masoko yapatikanayo katika Kaunti hiyo.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akiongea katika afisi yake siku ya Jumatatu, Muga alifafanua umuhimu wa makundi miongoni mwa wakulima wa samaki huku akidokeza kuwa kujiweka vikundi huleta ukomavu na kuimarika kwa bei ya samaki ambayo alitaja kuwa ya kuyumbayumba haswa katika Kaunti ya Kisii.

"Wakulima binafsi wamekuwa wakiyumbisha bei kwa sababu isiyoeleweka na kwa hiyo makundi huwa rahisi kuweka bei maalum ya kuuza samaki sokoni,” alisihi Muga.

Aidha Mkurugenzi huyo aliwaomba wakulima wa samaki kutoka Kaunti hiyo kushiriki kwenye hafla za mafunzo ambazo huandaliwa na idara yake kila wiki ambapo alidokeza kuwa wameanza makongamano ya kufundisha yeyote aliye na ari ya kufuga samaki katika eneo hilo la Gusii pamoja na maeneo ya Nyanza kusini.

“Tupo tayari na wazi kwa wakulima wetu ambao wamejitokeza na kuonyesha moyo wa kuendeleza kilimo hicho cha samaki,” aliongezea Muga.

Muga alisema kuwa wanalenga kupandisha idadi ya wakulima kutoka idadi ya takriban 2,000 ya sasa hadi zaidi ya 5,000 na zaidi alichukua nafasi yake kupongeza wakulima binafsi na makundi ambao wamekuwa wakutembelea ofisi zao kila siku ili kupata utaalam wa kufuga samaki.