Wafugaji wa ng’ombe katika mji wa Kisii na viungani vyake sasa watachukuliwa hatua kali za kisheria kwa kuwaacha mifugo wao kurandaradara katika barabara zilioko mjini humo na kutatiza shughli za usafiri.
Hii ni baada ya serikali ya kaunti kuanzisha mahakama ya kaunti ambayo itakuwa ikishughulikia kesi za aina hiyo na zingine nyingi.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu mjini Kisii, waziri wa ardhi na miji Moses Onderi alisema wale ambao wanafuga ng’ombe mjini humo na kuwaacha kurandaranda sasa watafikishwa katika mahakama ya kaunti na kushtakiwa kwa makosa ya kutojali mifugo wao na kutatiza shughuli za uchukuzi.
Kulingana na waziri huyo, sheria ya Kenya hairuhusu mifugo kufugwa katika miji mikuu.
“Kuna ng’ombe wengi ambao hurandaranda katika barabara za mji wa Kisii na viunga vyake na kutatiza uchukuzi, na tumekuwa tukipokea malalamishi hayo kwa muda mrefu sasa ng’ombe hao watachukuliwa na serikali ili mwenyewe ajitokeze na atashtakiwa,” alisema Onderi.
Wahudumu wa matatu na wanabodaboda wamekuwa wakilalamikia kurandaranda kwa mifugo hao kwa muda mrefu sasa na hii itakua afueni kwao.