Kamishna wa Kaunti ya Lamu Gilbert Kitiyo akiwahutubia wanahabari hapo awali. [Photo/ barakafm.org]
Kamishna wa Kaunti ya Lamu Gilbert Kitiyo ameagiza wafugaji wote wageni kuondoka kutoka kaunti hiyo.Akizungumza katika kikao na wanahabari siku ya Alhamisi, Kitiyo alisema muda ambao wafugaji hao walikuwa wamepewa umeisha na kuwataka kutii agizo hilo.Haya yanajiri baada ya baadhi ya wafugaji hao kushukiwa kuhusika katika mashambulizi ya kigaidi yaliyoshuhudiwa katika kaunti hiyo.“Tumegundua kuwa mauaji mengi hutokeo wakati wafugaji wanapohamahama,” alisema Kitiyo.Wiki iliyopita, Kitiyo alitoa agizo kwa machifu kuandikisha majina ya wenyeji wanaojihusisha na ufugaji, ili kurahisisha kazi ya kuwatumbua wageni.Kitiyo amesema kuwa iwapo wafugaji hao watakaidi amri hiyo, itailazimu idara ya usalama kutumia mbinu nyingine inayoambatana na sheria kuwafurusha.Aidha, Kitiyo amewaonya wakaazi dhidi ya kuingia katika msitu wa Boni, huku akisema kuwa hatua hiyo inahatarisha maisha yao.Kamishna huyo amesema kuwa sharti wakaazi hao watoe nafasi kwa maafisa wa KDF kukamilisha oparesheni yao ya kulipua msitu huo.Haya yanajiri siku moja baada ya watu wanne kuuawa na washukiwa wa al-Shabaab katika kijiji cha Hindi.