Wafugaji wa ng’ombe na mbuzi katika eneo la Utange, wamezitaka serikali za kaunti katika ukanda wa Pwani kupitia Idara za Kilimo, kuanzisha mradi wa kuwatibu mifugo wao hasaa msimu huu wa mvua.
Wakulima hao walisema kuwa mifugo wao hukumbwa na magonjwa mbalimbali wakati wa mvua.
Walisema kwamba hapo awali, serikali ya Kaunti ya Mombasa chini ya idara husika iliwatembelea na kuwatibu mifugo wao na kisha kuwaahidi kurudi na majibu ya uchunguzi wa baadhi ya sampuli walizochukua.
Kulingana na Moses Chiloh, maafisa wa maabara ya serikali ya Kaunti ya Mombasa walijukumika vilivyo kwa kutoa huduma za afya kwa mifugo hao.
Chiloh alisema kuwa juhudi sawia na hizo zinastahili kutekelezwa katika eneo nzima la Pwani, ili kuinua kilimo cha mifugo.
“Serikali za kaunti Pwani zinafaa kuiga mfano wa Kaunti ya Mombasa kwa kuanzisha mradi wa kuwatibu mifugo ulioanzishwa na kaimu mkuu wa Idara ya Kilimo Anthony Njaramba,” alisema Chiloh.
Akizungumza afisini mwake siku ya Jumatano, kaimu mkuu wa Idara ya Kilimo Anthony Njaramba alisema kuwa wakati wa Wapwani kukumbatia kilimo umefika.
“Kila kaunti inafaa kutoa huduma za matibabu kwa wakulima ili kuwapa motisha kuendelea na shughuli za ufugaji ambazo zinakumbwa na matatizo si haba katika eneo la Pwani,” alisema Njaramba.
Kwa upande wa magonjwa yanayowakumba mifugo hao, Njaramba alisema kuwa idara yake itasimama na wafugaji kwa kuwapa mataibabu ya bure na hata kuwashauri namna ya kuwaepusha mifugo wao dhidi ya magonjwa yanayoambatana na mvua.