Gereza ni sehemu inayoaminika na wengi kama eneo la mateso na dhiki, ambapo wafungwa hupitia maisha magumu kutokana na makosa waliyofanya.

Share news tips with us here at Hivisasa

Katika miaka ya hivi karibuni, mambo yameanza kubadilika huku serikali pamoja na mashirika mbalimbali wakianzisha miradi inayotoa matumaini ya maisha ya baadae kwa wafungwa.

Zaidi ya wafungwa 100 katika Gereza la Shimo la Tewa, Mombasa, walifuzu katika masomo ya dini na afya yaliyoandaliwa na kanisa moja eneo hilo.

Wafungwa hao wamekuwa wakifanya masomo hayo kwa muda wa kipindi cha miezi mitatu kwa ufadhili wa kanisa la SDA.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumamosi wakati wa hafla hiyo, mchungaji Rosena Kilimali wa kanisa la SDA, alisema wanalenga kusaidia wafungwa katika maisha yao ya baadae watakapotoka gerezani.

“Wafungwa wamehitimu katika jela hii ambapo tumekuwa tukiwafunza masomo ya Biblia na afya, na kila mtu amepokea cheti cha Diploma,” alisema Kilimani.

Kilimani aliongeza kuwa wanataka kubadilisha dhana iliyoko katika jamii kwamba wafungwa ni watu wasiofaa katika jamii, huku akisisitiza kwamba watu hao wanaweza kuwa muhimu zaidi katika familia zao baada ya kumaliza vifungo vyao.