Share news tips with us here at Hivisasa

Wakaazi wa Lokesheni ya Mochenwa wadi ya Gesima, eneo bunge la Kitutu Masaba, wameombwa kushirikiana ili kumaliza wizi na pombe haramu katika eneo hilo.

Akiongea siku ya Jumatano  katika hafla ya baraza katika uwanja wa shule ya Msingi ya Nyabiosi, lokesheni ya mochenwa, chifu wa lokesheni hiyo Magara Makori aliwaomba wakaazi wote kushirikiana ili kumaliza wizi na pombe haramu.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya chifu Magara kwa ushirikiano na naibu wake kumwaga zaidi ya lita 50 za chang’aa na zaidi ya lita 80 za busaa katika lokesheni hiyo na kuapa kuendelea kupiga vita pombe hiyo haramu.

Aidha, Magara alisema kuwa yeye kama afisa wa serikali, hatalala kamwe hadi ahakikishe kuwa pombe na wizi umeisha katika lokesheni hiyo.

“Mimi kama chifu nitahakikisha kuwa pombe katika lokesheni yangu  imeisha na vijana wanaotekeleza uwizi wamekamatwa na kuchukuliwa hatua ya kisheria," alisema Magara.

Chifu Magara aliwaomba wazazi kuwachunguza wanao kwa kile wanachofanya  na kubaini kazi wanaofanya kwani  uwizi umekita mizizi na vijana ndio wanalaumiwa sana.

“Naomba kila mzazi kujua kazi ambayo mtoto wake anafanya kwani vijana ndio wanalaumiwa sana katika wizi unaofanyika katika lokesheni yetu,”aliongezea chifu Magara.

Kulingana na chifu huyo, pombe katika lokesheni hiyo ndio huchangia kwa wizi kwani watu huiba ili kupata pesa za kununua pombe.

Wakaazi waliohudhuria hafla hiyo walisema kuwa ni lazima washirikiane pamoja kama wakaazi na kushirikiana na chifu ili kuhakikisha kuwa maovu katika lokesheni hiyo yameisha.