Wagema watano kutoka maeneo ya Kithyolo na Mbembani katika kaunti ndogo ya Yatta wametiwa mbaroni usiku was kuamkia Jumamosi katika msako dhidi ya pombe haramu,
Kwa mujibu wa Chifu wa kata ya Kithimani Josphat Kyalo Sila, alishirikiana pamoja na maafisa was polisi kutoka kituo cha polisi cha Matuu pamoja na viogozi wa nyumba kumi kuongoza operesheni hiyo.
Katika operesheni hiyo, chifu huyo alisema kuwa walinasa lita mia mbili za pombe haramu, na kuelezea kuwa wagema waliosalia na ambao bado hawajatiwa mbaroni wajue kuwa chuma chao ki motoni kwani operesheni za aina hii atazifanya mara kwa mara.
"Yeyote anayejihusisha na uuzaji au kupika pombe haramu ajichunge sana kwani hivi karibuni huenda akajipata taabani," alisema Sila.
Washukiwa hawa wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kithimani, na huenda wakafikishwa mahakamani hii leo, Jumatatu.