Share news tips with us here at Hivisasa

Mombasa inaendelea kushuhudia idadi kubwa ya wageni kutoka maeneo ya bara na sehemu zingine za Kenya wakiwa na hamu ya kutaka kuzuru mji huo wenye umaharufu mkubwa duniani haswa wakati huu wa sherehe za krisimasi.

Kila mwaka watu kutoka maeneo mbalimbali ya taifa hili huzuru mji huo kutokana na sifa wanazozipata kupitia vyombo vya habari na hali hiyo huwaongezea tamaa ya kutaka kuzuru japo mara moja tu.

Mwandishi huyu aliongea na Daniel Wafula katika kituo cha mabasi cha Mwembe Tayari mjini humo siku ya Jumamosi baada ya kufika kutoka mjini Busia akiwa na familia yake na kueleza sababu zilizomfanya kuchagua Mombasa.

“Hii ndio mara yangu ya kwanza kuja Mombasa, na sababu nimechagua hapa ni kwamba nimekuwa nikisika tu ikisifiwa sasa leo nimeamua kuleta familia yangu,” alisema Wafula.

Licha ya kwamba watu wengi wanaotoka maeneo ya bara na sehemu zingine za Kenya huamini kwamba gharama ya hoteli huwa juu wakati huu wa sherehe, wageni wengi waliozuru eneo hilo wiki hii wameusifia mji huo kutokana na mandhari yake.

Utafiti uliofanywa na mwandishi huyu katika hoteli kadhaa mjini humo ni kwamba bei ya chini ya kulala katika hoteli ni shilingi 1,000 hadi 5,000 usiku mmoja, huku zile za kifahari zikifika hadi shilingi 30,000.

Hata hivyo wenye hoteli tayari wameanza kuweka bajeti ya kunua vinywaji na vyakula mbalimbali ili kuwahudumia wageni wanaozidi kumiminika.