Hatimaye wakazi wa kaunti ya Nyamira ambao wamekuwa na ugumu wa kupimwa na kupokea matibabu ya ugonjwa wa sukari wamepata sababu ya kutabasamu baada ya wataalamu wa ugonjwa wa sukari kufanya hafla ya kuwapa matibabu kwenye uwanja wa shule ya msingi ya Nyamira.
Akihutubu kwenye shule ya msingi ya Nyamira wakati wa hafla ya siku mbili, naibu mkurugenzi wa masuala ya kliniki kwenye hospitali kuu ya Kenyatta Dkt Simon Monda amesema kuwa visa vya ugonjwa wa sukari husababishwa na mazoea ya kula vyakula vilivyo na sukari nyingi, kuwa na mawazo na hata pia kurithiwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
"Ugonjwa wa sukari husababishwa sana na mazoea ya kula vyakula vilivyo na sukari nyingi, watu kuwa na msongamano wa mawazo na hata pia hali ya kizazi kimoja kurithi kutoka kwa kizazi kingine," alisema Monda.
Afisa huyo aliongeza kwa kusema kuwa asilimia 60% ya wagonjwa wanaopewa uhamisho kutoka hospitali za kaunti mbalimbali hadi kwenye hospitali kuu ya Kenyatta haifai, kwa kuwa matatizo yao yanaweza kutatuliwa kwenye hospitali za kaunti kwa kuwa hospitali hizo zina uwezo wa kushughulikia matatizo hayo .
"Asilimia 60% ya wagonjwa wanaopewa uhamisho hadi hospitali kuu ya Kenyatta ni visa ambavyo vinaweza kukabiliwa kwenye hospitali za kaunti kwa kuwa sasa hospitali hizo zina uwezo wa kushughulikia matatizo hayo," alisema Monda.
Kwa upande wake mkurugenzi wa matibabu kwenye kaunti ya Nyamira Dkt Jack Magara alisema kuwa serikali ya kaunti imechukua hatua hiyo ili kuhakikisha kwamba watu wa maeneo hayo wanapata kupimwa mara kwa mara bila malipo, huku akiongeza kusema kuwa watu wengi walijitokeza kupimwa.
"Serikali ya kaunti hii ilichukua hatua hii ya kuwapima wakazi ili kuhakikisha kuwa watu wengi wasio na uwezo wa kuenda kupimwa ili kubaini iwapo wameathiriwa na ugonjwa wa sukari wamepata nafasi ya kufanya hivyo," aliongezea Magara.