Tangu kuanzishwa kwa msako wa kuwatafuta wahalifu jijini Mombasa, idara ya usalama katika kaunti imefanikiwa kuwaua kwa kuwapiga risasi wahalifu kumi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Maalim Mohamed amesema kuwa wahalifu hao walikuwa sugu na walikuwa wakiwahangaisha wakaazi mara kwa mara.

Akizungumza siku ya Ijumaa, Maalim alisema kuwa sita kati yao waliuawa katika gatuzi dogo la Nyali na Kisauni, huku wawili wakiwa ni washukiwa wa ugaidi waliouawa katika eneo la Junda-Mishoroni mwezi uliopita.

Kamishna huyo alisema kuwa majambazi hao wengine wawili waliuawa siku ya Jumapili katika maficho yao eneo la KCC Miritini.

Maalim amesisitiza kuwa kamwe juhudi zao za kuimarisha usalama kwa Wakenya hazitatatizwa na viongozi wanaowashutumu kwa kutekeleza mauaji ya kiholela.

“Maafisa wa polisi wataendelea kuwakabili wahalifu vilivyo ili kuhakikisha usalama unaimarishwa Mombasa,” alisema Maalim.

Haya yanajiri baada ya Gavana wa Mombasa Hassan Joho pamoja na Mbunge wa Kisauni Rashid Bedzimba kuwakashifu maafisa wa polisi kwa kutekeleza mauaji ya washukiwa wa uhalifu.

Viongozi hao walisema kuwa sharti wahalifu wakamatwe na kufikishwa mahakamani badala ya kuuawa kiholela.