Idara ya Usalama Kaunti ya Mombasa imesema inaweka mikakati ya kuwanasa vijana wanaowatishia wenyeji eneo la Soko Mjinga kule Kisauni.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kupitia kwa Kamishna Mkuu Kaunti ya Mombasa Bw Mohammed Maalim, idara hiyo imesema tayari mchakato wa kuanzisha msako wa makundi yanayotekeleza uhalifu eneo hilo umeanza huku maafisa wa polisi wakitarajiwa kushika doria mchana na usiku.

Akizungumza na waandishi wa habari, Maalim amesema kuwa eneo hilo limekuwa hatari kwa usalama wa mwananchi na akatoa mfano wa mauaji ya hivi majuzi yaliyosababishwa na kundi linalojiita Wakali Kwanza.

Aidha, Maalim amesema maafisa wa usalama watachunguza mienendo ya vikundi vya vijana vinavyotembea pamoja nyakati za usiku na mchana ili kupata taarifa kamili ya namna kundi la Wakali Kwanza linavyoendesha shuhhuli zake za kikatili.

Aliongeza kudokeza kuwa operesheni hiyo haitakuwa ya eneo la Soko Mjinga pekee bali maafisa hao watasambazwa kote Kisauni hadi maeneo ya Mshomoroni ambako kunaaminika kuwa maficho ya kundi hilo.

Hata hivyo amewataka wakazi wa eneo hilo kushirikiana na maafisa wa usalama ili kufanikisha oparesheni hiyo.