Vijana wawili kutoka mtaa wa Kibera ambao wamekuwa miongoni mwa magaidi wanaosakwa sana na polisi walijiwasilisha kwa polisi pamoja na silaha ambazo wamekuwa wakizitumia.
Wawili hao walijiwasilisha siku ya Jumapili kwa OCPD wa Kilimani, Peter Kattam na bunduki mbili aina ya pistol, mojawapo ikiwa bunduki bandia, ambazo wamekuwa wakitumia kuwahangaisha watu.
‘‘Nawashukuru vijana hawa kwa uamuzi walioufanya. Uhalifu hauna umuhimu wowote na kitendo hiki kitawawezesha vijana hawa kuishi maisha marefu kwa sababu wangezidi kuwa katika uhalifu basi wangeuwawa mapema,’’ alisema Kattam.
Wawili hao walikiri kutekeleza uhalifu katika maeneo mbalimbali jijini Nairobi ikiwemo maeneo ya Lang’ata, mtaa wa Kibera na Karen.
Kattam amewataka vijana wengine 32 wanaosakwa kujiwasilisha pia kwa polisi huku akitoa wito kwa vijana wengine kukoma kujihusisha na ugaidi na kuonya kuwa chuma chao ki motoni.
‘‘Ningewaomba vijana wengine 32 ambao wanamiliki silaha hatari ziwe bandia wajiwasilishe kwa polisi kwani tuko tayari kuja katika mtaa wa Kibera kila wikendi kusheherekea mabadiliko ya vijana wetu na kuchukua silaha,’’ alisema Kattam.
Kattam alisema kuwa iwapo vijana wanaohusika na uhalifu haswaa katika mtaa wa Kibera watajiwasilisha kwa vyombo vya usalama basi hakutakuwepo na visa vya uhalifu katika mtaa huo. Aliongeza kuwa vijana hao watapewa fursa ya kubadili maadili waliokuwa nayo mabaya.