Mwalimu wa Shule ya msingi ya Mageri iliyoko katika wadi ya Bomwagamo, Kaunti ya Nyamira, amewaomba wahisani kumsaidia kujenga afisi yake iliyoko kwenye hatari yakuporomoka.
Akiongea na wanahabari nje ya afisi yake siku ya Alhamisi Ezekiel Nyakamba alisema kwamba kwa muda sasa kamati ya ujenzi ya shule hiyo imekuwa ikijaribu kutafuta usaidizi kutoka kwa hazina ya CDF ya eneo bunge la Mugirango Kaskazini bila mafanikio.
"Tumekuwa tukijaribu kutafuta msaada wakujenga afisi kuu kutoka kwa hazina ya CDF katika bunge hili bila mafanikio, na sasa tunahitaji msaada wa wahisani ili kukarabati afisi hii," alisema Nyakamba.
Mwalimu huyo alisema kuwa shule hiyo inahitaji shillingi laki mbili unusu ili kukarabati afisi hiyo inayo nakisiwa kujengwa miaka ya sabini.
"Tunahitaji msaada wa Sh250,000 ili kukarabati afisi hii kwa maana sasa imechakaa na iko kwenye hatari yakuporomoka,” alisema Nyakamba.
Haya yanajiri baada ya paa la darasa la nane kwenye shule hiyo kuanguka miezi miwili iliyopita kutokana na upepo mkali uliosababisha hata upande mmoja wa kuta za darasa hilo kuporomoka.