Baadhi ya Wahubiri wa Kanisa la Full Members lilioko eneo la Egesa Wilayani Kisii ya Kati eneo Bunge la Kitutu Chache Kusini, Kaunti ya Kisii wamewaomba Wabunge kukana ndoa ya Jinsia moja kutokubaliwa humu nchini.
Akiongea siku ya Ijumaa katika shirika liliokuwa likifanyika katika eneo hilo la Egesa, Daniel Ochoi ambaye ni Mhubiri wa Kanisa hilo alisema kuwa ndoa ya jinsia moja isikubaliwe kamwe nchini huku akiwaomba Wabunge kutokubali kwani kitendo hicho ni kinyume na Bibilia.
Ni siku chache tu baada ya Mahakama Kuu nchini kuwakubalia baadhi ya watu wanaotaka ndoa ya jinsia moja kuwa na chama chao ambacho wengi wa wananchi haswa Wahubiri wamekilaani baada ya kutofurahishwa na uamuzi huo wa Mahakama Kuu.
Wakati uo huo, Mhubiri huyo alisema ni kinyume na Bibilia na hata na utamaduni wa Mwafrika kuwa na ndoa ya jinsia moja jambo ambalo walikitaja kitaleta laana kwa watu.
“Ni sisi tunajiua wenyewe wakati ndoa ya jinsia moja inatakiwa kuanzishwa humu nchini. haipaswi sisi kama watumishi wa Mungu pamoja na Wabunge kuyakubali mambo kama haya katika jamii,” alisema Fredric Ombwori ambaye pia ni Mhubiri wa Kanisa hilo.
Aidha, Wahubiri hao waliunga mkono matamshi ya Naibu Rais William Ruto ambaye alikana kuwa ndoa hiyo haitakubaliwa nchini Kenya huku wakiwaomba viongozi wengine kuungana na Ruto kufutilia mbali mahitaji hayo ya kuwa na ndoa ya jinsia moja nchini.
“Heri tumwombe Mungu usiku na mchana huku tukilaani ndoa hiyo kwani mwanaume aliumbwa katika shamba la Edeni waoane na mwanamke. Haya ya kuoana mwanaume kwa mwanamme yalitoka wapi tena jamani?,” auliza Mhubiri Ombwori.