Takribani wahudumu sitini wa tuktuk wamekamatwa na maafisa wa trafiki kwa makosa mbalimbali ikiwemo ya kuendesha magari hayo bila vibali.
Akizungumza siku ya Ijumaa na wanahabari katika afisi yake, kamanda wa trafiki wa Kituo cha polisi cha Central Shem Omolo, alisema kuwa msako huo uliaanza kufuatia visa mbalimbali vya kila mara vya ajali zinasababishwa na madereva wa tuktuk.
“Msako huu ambao ulianzishwa siku ya Ijumaa utaendelea hadi pale visa vya ajali vitakapopungua kwa kiasi cha kuridhisha katika Kaunti ya Mombasa,” alisema Omolo.
Hata hivyo, juhudi za wamiliki wa tuktuk kuwaondoa wafanyakazi wao katika kituo hicho ziligonga mwamba kwani wengi wa waliokamatwa walipatikana kuwa hawana leseni za kuendesha magari hayo katikati mwa mji wa Mombasa.
Omolo alisisitiza kuwa madereva hao watafikishwa mahakamani kujibu shtaka la kukiuka sheria za trafiki.