Naibu wa gavana wa kaunti ya Kisii, Joash Maangi, amewahakikishia wahudumu wa afya katika kaunti hiyo kwamba serikali ya kaunti itaendelea kuangalia maslahi yao na kuweka mazingira mema ya kufanyia kazi.
Akizungumza katika kikao na wauguzi na viongozi wao, katika chumba cha mikutano cha St Vincent mjini Kisii, Maangi amesema kuwa serikali ya kaunti inatambua kazi ambayo wauguzi hao wanafanya.
Aliongeza kwamba kazi ya waaguzi hao ndio imepelekea kaunti ya Kisii kuwa ya kwanza nchini katika huduma za matitbabu.
Aidha, naibu huyo wa gavana aliwasifu viongozi wa chama katika kaunti hiyo kwa kufanya mashauriano na serikali ya kaunti.
Aliwasifia pia kwa kutumia njia ya kidemokrasia bila kuitisha migomo kama ilivoshuhudiwa katika kaunti nyinginezo.
Maangi amesema haya siku chache baada ya wahudumu wa afya kwenye kaunti hiyo kulalamikia mazingira mabaya ya kufanya kazi na uhaba wa wauguzi.
Kwa ujumla sekta ya afya nchini imekuwa ikikumbwa na changamoto kama vile migomo ya wahudumu wa afya ambayo husababishwa na mishara midogo, kukosa kupandishwa vyeo na kucheleweshwa kulipa mishahara.