Wahudumu wa afya kaunti ya Lamu siku ya Jumatatu. /NMG
Wahudumu wa afya kutoka kaunti ya Lamu waliandamana siku ya Jumatatu na kupinga vikali kuwa wamekuwa wakiwasaidia wapiganaji wa kundi la Al-Shabaab kupata matibabu na pia dawa.
Wahudumu hao kutoka vituo kadhaaa vya afya kaunti ya Lamu waliandamana na kupeleka lalama zao katika afisi ya kamishna wa kaunti ya Lamu Gilbert Kitiyo na kutaka kuachiliwa huru kwa wenzao ambao walikamatwa wiki iliyopita na pia mashtaka dhidi yao kuondolewa baada ya kudaiwa kuwa walikuwa wakiwapatia magaidi wa Al-Shabaab dawa pamoja na kuwatibu.
Wakiongozwa na mwenyekiti wao Daktari Ahmed Farid, waandamanaji hao walisema kuwa wanahitaji kuheshimiwa na kuachwa kunyanyaswa na serikali ya kitaifa.
Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na uvumi kuwa dawa zimekuwa zikipelekewa wapiganaji wa Al-Shabaab na pia baadhi ya wahudumu wa afya wamekuwa wakiwatibu.