Ongezeko la ajali za barabarani zinazohusisha pikipiki huchangiwa na hatua ya wahudumu wa bodaboda kuingilia biashara hiyo kabla ya kutimiza kanuni zote za idara ya trafiki.
Haya yamefichuka kwenye mkutano wa wahudumu wa pikipiki katika eneo la Keringet wilayani Kuresoi ambapo maafisa wa trafiki wamewafanyia ukaguzi baadhi ya madereva hao ili kujua jinsi walivyohitimu kuendesha pikipiki.
Kinyume na madaha ambayo wengi wao hutumia wakiendesha pikipiki, ujanja wao umeonekana kuishia jangwani baada ya kukosa kufaulu katika mazoezi mbali mbali mbele ya maafisa wa trafiki.
Kamanda wa polisi eneo hilo David Wambua amesema wengi wa wahudumu wa bodaboda hawana leseni licha ya kuwa wakihudumu na kubeba abiria.
Wambua amesema vijana hao ambao wengi wao ni wenye kati ya miaka 19-40 hujitoza katika biashara hiyo baada ya kujifunza kuendesha pikipiki kwa siku kadhaa kwenye barabara za mashambani jambo ambalo linachangia ongezeko la ajali za pikipiki.
Wambua amesema licha ya uchukuzi wa pikipiki kutumika kwa wingi kama njia ya usafiri katika maeneo mbali mbali, sekta ya bodaboda imegeuka kuwa chanzo cha mauti za mapema kwa wasafiri na wahudumu wake kufuatia mikasa barabarani.
Takwimu zimedhihirisha kwamba ajali zinazohusisha pikipiki zinaendelea kuongezeka huku idara ya trafiki ikijizatiti kuhakikisha wahudumu wa pikipiki wameheshimu sheria na kanuni za trafiki ili kupunguza maafa zaidi.
Kwa mujibu wa afisa huyo ongezeko la ajali zinazohusisha pikipiki husababishwa na wahudumu kukosa kuafikia malengo yote ya idara ya trafiki kabla ya kuingilia sekta ya uchukuzi wa pikipiki.
Riporti ya shirika la afya duniani (WHO) kuhusu usalama barabarani ya mwaka elfu 2013 ilisema kando na magari, pikipiki husababisha idadi kubwa ya ajali za barabarani katika mataifa yanayostawi, maafa ambayo lazima yadhibitiwe.
Edward Kiprotich ambaye huuza vihasho(spares) vya pikipiki amesema uchukuzi wa pikipiki nchini ulishika kasi kama mbinu ya usafiri wa umma miaka 13 iliyopita, pale serikali ilipoondoa ushuru uliokuwa ukitozwa waagizaji wa pikipiki na baiskeli pamoja na kodi iliyokuwa ikitozwa pikipiki za injini ya kiwango cha chini kama vile 250cc.
Mfanyibiashara huyo amesema hatua hiyo ya serikali ilipiga jeki sekta ya bodaboda na kuwapa vijana nafasi ya kupata ajira huku idadi ya pikipiki zilizosajiliwa nchini ikiendela kuongezeka kila mwaka.
Licha hayo pikipiki zimeondokea kupendwa na watu wengi kwa sababu huwafikisha abiria wake hadi mahali wanapotaka.
Hata hivyo serikali imetakiwa kuweka mikakati mathubuti kwenye sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kuanzisha shule maalum za kutoa mafunzo ya uendeshaji pikipiki katika kila jimbo.
Aidha imearifiwa kuwa majeruhi wa ajali za pikipiki wamekuwa changamoto kubwa katika hospitali nyingi za umma kuona baadhi ya vituo vya afya vimetenga wadi maalum za kushughurikia waadhiliwa wa ajali za pikipiki.