Mkuu wa polisi katika kaunti ndogo ya Kikuyu Jumanne aliwaonya wanabodaboda dhidi ya unajisi wa watoto kufuatia visa vingi vilivyoripotiwa kwa muda wa mwezi mmoja sasa.
Hii ni baada ya mhudumu mmoja wa bodaboda katika eneo la Zambezi kuepuka kifo baada ya kuvamiwa na umma kwa madai ya kumnajisi msichana wa miaka kumi na miwili.
Akidhibitisha hayo katika ofisi yake, OCPD wa eneo hilo Mutune Maweu alisema kuwa visa vya watoto kunajisiwa na wahudumu wa bodaboda vimekuwa vingi kaunti ya Kiambu.
Alisema kuwa kwa muda wa mwezi mmoja, visa ishirini na moja vimeripotiwa kutoka sehemu mbali mbali za kaunti ndogo ya Kikuyu.
Kulingana na mkuu huyo wa polisi, maeneo ya Kinoo na Kikuyu ndiyo yameripoti idadi kubwa ya visa hivyo.
"Visa kama saba vimefanyika na kuwaacha watoto wachanga wakiwa wajawazito. Nataka kuwaonya wahudumu wa boda boda dhidi ya tabia hii na yule atayekamatwa atashtakiwa vilivyo," alisema Maweu.
Aidha Maweu aliongeza kwamba machifu na manaibu wao wamesaidia katika oparesheni ya kuwatia mbaroni wahusika.
Inadaiwa wahudumu wa bodaboda huwadanganya watoto kwa peremende.
“Nawaomba wakaazi wote wawe macho ili kuwalinda watoto wetu dhidi ya unyama huu,” aliongeza mkuu huyo wapolisi.