Wahudumu wa bodaboda katika eneo la Kisauni wamefanya maandamano kulalamikia hatua ya maafisa wa polisi kuwahangaisha nyakati za usiku.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wahudumu hao walisema kuwa maafisa hao huwasingizia kuwa wanahusika katika visa vya uhalifu.

Walisema kuwa zaidi ya wenzao watano wamekamatwa na maafisa wa polisi baada ya kupatikana kwenye sehemu ya maegesho saa tatu usiku wakiendelea na kazi zao.

Kulingana na Omar Chibwa, mhudumu wa pikipiki, maafisa wa polisi hutembea eneo hilo kila usiku na kuwakamata.

Chibwa alisema kuwa idara ya usalama katika Kaunti ya Mombasa haijatoa onyo la wakati wa kufanya kazi kwa wahudumu hao.

“Hatua ya maafisa inahujumu kazi yetu kwani kila mwananchi ana haki ya kufanya biashara wakati wowote hapa nchini,” alisema Chibwa.

Shikali Denno, mhudumu wa pikipiki, alisema kuwa alikamatwa na polisi licha ya kutokuwa na hatia.

“Maafisa wa polisi walinikamata kwa kisingizio kuwa nilipatikana na dawa za kulevya. Mimi sio mtumizi wa mihadarati wala sijawahi kujihusisha na biashara hiyo,” alisema Shikali.

Haya yanajiri baada ya idara ya usalama kusema kuwa baadhi ya wahudumu wa pikipiki na tuktuk katika eneo la Kisauni wanashirikiana na vijana ikutekeleza maovu kwenye mitaa mbalimbali kama vile ya Katisha na Frere Town.

Hata hivyo, wahudumu hao wamewataka maafisa wa polisi kufahamu kuwa sio wahudumu wote wanaojihusisha na dawa za kulevya na uhalifu.