Wahudumu wa bodaboda katika eneo la Kisauni wameonyesha kugadhabishwa na hatua zinazochukuliwa na idara ya usalama kuhakikisha kuwa hali ya usalama inadumishwa katika eneo hilo.
Wakizungumza siku ya Jumamosi katika kituo cha kuegesha pikipiki cha Freretown, wahudumu hao ambao hawakutaka kutajwa walidai kwamba maafisa wa usalama huwasimamisha nyakati za usiku, na kuwatafutia na hata kuwaekea makosa.
Wahudumu hao walidai kuwa maafisa hao wa polisi wanania ya kuwahusisha na visa vya utovu wa usalama, kwasababu hawana taarifa zozote kuhusiana na makundi ya uhalifu.
Wahudumu hao aidha wamesema kwamba tangu kijana mmoja aliyehusishwa na kundi la kihalifu la Wakali Kwanza kuuawa, kumekuwepo na uchunguzi wa mara kwa mara katika eneo hilo ambapo wengi wao wanajipata kubanwa na maswali yasiyoeleweka na maafisa wa usalama.
Aidha, walisema kuwa kwa sasa kunamadai kuwa wahudumu wa bodaboda wanawafahamu wahalifu wa eneo hilo, jambo ambalo wamelikana na kuwataka maafisa wa usalama kuendesha uchunguzi wao kwa njia halali.
Walisema kuwa atakayepatikana na hatua anapaswa kuchukilwa hatua za kisheria.