Wahudumu wa pikipiki katika eneo la Kisimani wameapa kushirikiana na maafisa wa polisi kuyasaka makundi ya wahalifu yanayoendelea kuwa kero kwa wakaazi wa eneo hilo.
Wahudumu hao waliojawa na ghathabu walisema kuwa kuna makundi ya vijana yanayojuhusisha na uhuni, hatua iliyosabababisha athari nyingi kwa wahudumu hao, ikiwemo wizi wa pikipiki na mauaji ya kiholela.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa wahudumu wa pikipiki katika kituo cha Kisimani Jamal Rama, wahudumu hao walisema kwamba tayari wamefikisha malalamishi yao kwa mwakilishi wa wadi wa eneo hilo Bwana Amir Thoya.
Rama alisema kwamba kilichosalia sasa ni kuungana na maafisa wa usalama wanaoshika doria mchana na usiku eneo hilo, ili kuangmiza vitendo vya uhalifu vinavyozidi kuripotiwa kila uchao katika eneo la Katisha, Freretown, Kisauni na Kisimani.
Rama aidha ameongeza kwamba jumla ya wahudumu wa pikipiki 50 wa kituo hicho na wengine 20 kutoka eneo la Katisha wameapa kushirikiana na wenzao kutoka Kisauni ambao wamekuwa walengwa wakuu wa visa hivyo.
“Kila kunaporipotiwa visa vya uhalifu, wahidumu wa bodaboda ndio huwa wa kwanza kuhusishwa na visa hivyo. Jambo hilo ni kinaya kikubwa kwani pia wahudumu wamekuwa wakihangaishwa na kundi ya Wakali Kwanza, linaloaminika kutekeleza uhalifu Kisauni,” alisema Rama.