Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wahudumu wa bodaboda Likoni wamepewa makataa ya wiki moja kutafuta stakabadhi muhimu zinazohitajika kuendesha biashara hiyo.

Idara ya usalama imesema itaanzisha msako mkali wiki ijayo ili kuhakikisha kwamba wahudumu hao wanatimiza sheria.

Msako huo pia unanuia kukomesha utovu wa nidhamu miongoni mwa wahudumu hao.

Akizungumza katika kikao na wahudumu hao siku ya Jumatano, naibu kamishna wa Likoni Albert Kimanthi alisema amewapa wahudumu hadi siku ya Jumanne wiki ijayo kabla ya kufanya msako huo.

“Hivi vibali ni muhimu na mwafaa kuwa navyo. Hili silo jambo geni kwani nyote mnajua sheria hiyo. Tungeanza msako wetu leo lakini tunawapa muda mfupi wa kutafuta stakabadhi hizo,” alisema Kimanthi.

Kimanthi aliongeza kwamba wanataka kuwatambua wahudumu wote wa bodaboda eneo hilo, huku akiwahimiza wenyekiti wa vituo vya bodaboda kuwasisitizia wanachama wao umuhimu wa kufuata maagizo.

Akizungumzia kisa kilichotokea wiki jana ambapo wahudumu hao walidaiwa kuvamia kituo cha polisi cha Likoni, Kimanthi alisema hapakuwa na mawasiliano mazuri baina ya maafisa wa polisi na wale wa kaunti kuhusu jinsi ya kufanya msako huo.

Kimanthi amependekeza manaibu kamishna katika kila kaunti ndogo kupewa jukumu la kupanga siku na wakati wa kufanya misako ili kuepuka visa kama hivyo kutokea.

“Polisi walikuwa wanatekeleza jukumu lao lakini shida ni kwamba hatukupanga msako huo pamoja. Itakuwa vizuri kama kamati ya usalama itashirikiana kutekeleza majukumu yao,” alisema Kimanthi.

Wahudumu wa bodaboda waliunga mkono kauli hiyo, lakini wakawalaumu maafisa wa polisi kwa kuwahangaisha kila wanapoweka mikakati ya kuendesha biashara zao.

Richard Mbuvi, mmoja wa wahudumu hao, alisema kwamba hapo awali walikuwa wameanzisha kibali maalum cha kutambulisha kila pikipiki na kituo kinachohudumu, lakini maafisa wa polisi wakapinga hatua hiyo.

“Tulikuwa tumeweka alama ya kutambulisha kama pikipiki ni ya the Office, Jamsa na kadhalika, lakini polisi wakasema tuchukue ile ya kaunti peke yake,” alisema Mbuvi.