Wahudumu wa pikipiki katika eneo la Freretown kaunti ya Mombasa wamewataka wenzao kuwa waangalifu wanapoendesha pikipiki haswa katika maeneo ya makazi.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakizungumza mapema leo katika kituo cha kuegesha pikipiki cha freretown, wahudumu hao wamesema walisikitishwa na kitendo ambapo muhudumu mwenziwao alimgonga mtoto mdogo mwenye umri wa miaka sita na kususia kusimama kama alivyotakiwa na wakazi wa eneo hilo.

Wahudumu hao aidha wamesema kuwa ni muhimu kwao kujua sheria zote za barabara na kuzizingatia pasi kuenda kinyume cha sheria hizo.

Mtoto huyo ambaye anasemekana alipatwa na mkasa huo alikuwa akielekea dukani baada ya kutumwa na mamake kwenye duka lililokaribu na nyumbani kwao.

Japhet Ondari, mhudumu wa pikpiki katika eneo hilo anasema kuwa mwenzao aliyekuwa ametoka upande wa kisimani alijaribu kumkwepa mtoto huyo lakini akashindwa kudhibiti uzito wa pikipiki hivyo basi kuishia kumgonga mtoto huyo japo hakupata majeruha mabaya baada ya kupigwa picha katika hospitali kuu ya kaunti ya Mombasa.

Wahudumu hao wamesema kuwa itawalazimu wao wenyewe kuweka matuta sehemu mbalimbali za barabara zote zinazoingia katika makazi ili kuepukana na visa vya ajali za mara kwa mara ambazo mara nyingi zinawahusisha watoto wadogo huku wakisema kuwa huenda mwenzao alikataa kusimama kwa kuogopa wakazi waliokuwa wanamfuata kwa gadhabu .

Hata hivyo wamemtaka mwakilishi wa wadi wa Freretown Amir Thoya kuwasaidia katika kusuluhisha kesi hiyo baina yao na familia ya mtoto aliyepata ajali hiyo.

Image caption. wahudumu wa bodaboda wakiwa katika kituo cha kuegesha pikipiki zao, wamekashifu kitendo ambapo mwenzao alimgonga mtoto mdogo na kutoroka.