Idara ya trafiki mjini Mombasa imewalaumu madereva wa pikipiki wanaohudumu kwenye maeneo mbalimbali mjini humo kwa ongezeko la ajali.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Idara hiyo imesema kuwa mara nyingi ripoti ya ajali inapotolewa kwa maafisa wa usalama wa barabarani, wanaopatikana kuhusika pakubwa ni wahudumu wa pikipiki.

Kulingana na Shem Omolo, kamanda mkuu wa trafiki katika kituo cha Central mjini Mombasa, wahudumu hao huhusika katika ajali hizo kutokana na kutozifahamu sheria za barabarani vyema.

Omolo alisema kuwa madereva wengi wa bodaboda hujifunza kuendesha pikipiki nyumbani, jambo ambalo alilitaja kuwa hatari kwa maisha ya wateja wao na madereva wenyewe.

“Wahudumu wengi hawazingatii sheria za barabarani na hata wanapoelekezwa na maafisa wa trafiki, wao huishia kupenya kwenye misongamano ya magari ambapo mara nyingi huishia kubanwa na magari kutokana na sehemu ndogo inayobakia baina ya magari yanapokuwa kwenye msongamano,” alisema Omolo.

Bwana Omolo pia amewataka vijana wanaoendesha bodaboda kuwa makini na kufuata sheria za barabarani.

Aidha, amewaonya wanaoendesha pikipiki bila liseni kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria.