Kulitokea kizaazaa kwenye kituo cha kibiashara cha Kibuye mjini Kisumu wakati wanaoendesha Bodaboda walipomkabili vikali kijana mmoja ambaye alipatikana akibeba abiria bila kuwa na kitambulisho cha kazi eneo hilo.
Waendeshaji Bodaboda hao ambao walijawa na hamaki walitishia kumpeleka kijana huyo kwenye kituo cha Polisi wakidai kwamba alikua ni mmoja miongoni mwa walaghai ambao huwaibia wafanyibiashara bidhaa zao sokoni humo na kusingizia wahudumu wa Bodaboda.
“Ninyi ndio mnatupaka matope na kudunisha kazi yetu. Tunataka kitambulisho cha kazi na pia utuambie unafanya kazi yako kupitia kikundi gani,” aliteta Mark Ochola mmoja wa wahudumu hao.
Kisa hicho kilizua utata wakati wamama walipoingilia kati kumtetea kijana huyo ambaye alianza kulia akisema kuwa anajitafutia riziki baada ya wazazi wake kufariki dunia mwaka mmoja uliopita na kukosa mtu wa kumpa mahitaji.
“Ninyi ndio wenye kulalama kwamba tunawaibia bidhaa zenu kwenye soko hili na ninyi ndio wa kwanza kumtetea mushukiwa,” wahudumu hao waliwakemea vikali wamama hao ambao wanafanya biashara kwenye soko hilo.
Aidha, wamama hao waliwataka wahudumu hao wa Bodaboda kumuachilia kijana huyo na kuwataka kila mmoja kuzingatia kazi yake, wakisema kuwa wanamhangaisha kijana huyo bila sababu na kwamba hafai kuhusishwa na wizi wa bidhaa kwenye soko hilo.
Kumekuweko na madai kwamba wahudumu hao huwaibia wafanyibiashara kwenye soko hilo mizigo ya bidhaa zao kwa kuhepa nazo wakati wanapowabebea kuingiza na kutoa sokoni.