Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wahudumu wa bodaboda katika Kaunti ya Mombasa wamelalamikia kudhulumiwa na baadhi ya maafisa wa polisi wa trafiki katika shughuli zao za kikazi.

Kulingana na wahudumu hao, kuna baadhi ya maafisa wa trafiki mjini Mombasa na maeneo ya Changamwe na Likoni, ambao huabiri bodaboda hizo kisha hukaidi kuwalipa nauli, huku wahudumu wengine wakitiwa nguvuni bila ya sababu zozote za kimsingi.

Wakiongea na mwanahabari huyu mjini Mombasa siku ya Jumatano, wahudumu hao wa bodaboda, wakiongozwa na mwenyekiti wao Alphan Mwatsahu walidai kwamba visa hivyo vya dhulma vinavyotekelezwa na maafisa wa polisi haswa wale wa trafiki vimekithiri mno katika kaunti hiyo na kuwatia hofu.

Aidha, walimtaka Kamanda mkuu wa trafiki pamoja na yule wa polisi kuingilia kati swala hilo na kuwaonya maafisa hao wa trafiki na wale wa polisi wanaoendeleza dhuluma hizo huku wakisema kwamba wahudumu hao wanahaki kikatiba.

“Tumechoka na dhulma za kila siku tunazofanyiwa na maafisa wa polisi wa trafiki kwa sababu hao huabiri bodaboda na ukiwaitisha nauli, inakuwa ugomvi kwani hawataki kulipa. Ukishindana nao, unatiwa nguvuni kisha unapelekwa kotini. Ukifika kotini, unaandikiwa umevunja sheria za barabarani,” alisema Mwatsahu.

Wahudumu hao waliahidi kuungana na wale wa tuktuk mjini Mombasa na kufanya maandamano ya kuishinikiza idara ya trafiki kuwaonya maafisa wao dhidi ya kuendeleza dhulma kwa wahudumu hao mjini Mombasa.