Wahudumu wa magari ya usafiri wa umma mjini Nakuru wanaitaka serikali ya kaunti kukarabati na kupanua steji kuu ya magari mjini Nakuru.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Katika mahojiano na mwandishi wetu, wahudumu hao wa matatu walisema kuwa hali katika steji hiyo imedorora huku nafasi ikizidi kuwa finyu kutokana na ongezeko la watu mjini.

Walisema kuwa ongezeko la watu mjini limepelekea kuongezeka kwa idadi ya magari ya usafiri wa umma, hali ambayo imepelekea kituo hicho kufurika kupita kiwango chake.

David Mathenge ambaye ni dereva wa magari ya kwenda mtaani Bahati alisema kuwa steji hiyo inahitaji ukarabati wa dharura kabla ya msimu wa mvua kuanza kwani imechimbuka vibaya.

“Gavana alituahidi kuwa hii steji ingekarabatiwa na kufanywa ya kisasa lakini hadi sasa haujaona dalili ya ukarabati kufanyika na huenda steji hii ikazidi kuharibika iwapo haitafanyiwa ukarabati. Itakuwa vigumu watu kuingia hapa wakati wa mvua iwapo haliitabakia kuwa hivi ilivyo,” alisema Mathenge.

Stanley Nyambane, ambaye pia ni dereva alisema kuwa msongamano wa magari katika steji hiyo unahatarisha maisha ya wasafiri kwani inakuwa vigumu kwa mtu kutoroka panapotokea dharura kutokana na uchache wa nafasi.

“Hapa kuna hatari kwa sababu kama kunaweza kutokea dharura watu wengi watajeruhiwa kwa kukosa nafasi ya kutorokea,” alisema Nyambane.

Mwenyekiti wa steji hiyo Stephen Nderitu alisema kuwa tayari wamewasilisha lalama zao kwa gavana na wanangojea majibu kutoka huko na kusema kuwa wana imani kuwa steji hiyo itafanyiwa ukarabati.

“Tumeongea na watu wa serikali na tumewambia kuwa tunataka kazi ifanyike hapa na tunatarajia kuwa watatujibu hivi karibuni kama walivyo ahidi,” alisema Nderitu.