Wadumu wa matatu katika barabara ya Eldoret-Kapsabet wameandamana mchana wa leo wakilalamikia kunyanyaswa na Maafisa wa Trafiki.
Maandamano hayo yamefanyika baada ya dereva mmoja aliyekuwa mtumwa wa maafisa hao kunaswa na takriban Sh70,000 asubuhi ya leo huku fedha hizo zikisemekana kuwa ni zile zinazotozwa wahudumu hao na maafisa hao.
Kulingana na Sosten Ruto ambaye ni katibu wa muungano wa wahudumu wa matatu katika Kaunti ya Uasin Gishu, ufisadi huo ambao amedai umeendelea kwa miaka mitatu sasa umewadhalilisha wanabiashara wa matatu ikizingitiwa kwamba maafisa hao huchukua Sh300 kwa kila gari kutoka kwa magari yote 150.
Katibu huyo ameongeza kwamba magari yote yanayohudumu chini ya muungano huo yametimiza mahitaji yote katika sheria za usafiri na kwamba maafisa hao wana uzoefu wa kukusanya fedha hata bila magari hayo kuwa na tatizo lolote huku akiomba tume ya kuwapiga msasa maafisa wakuu wa Polisi kuleta mabadiliko katika Idara hiyo inayozorota kila kuchao kutokana na ufisadi na baadhi ya Maafisa wengine.
Kwa upande wake mwenyekiti wa muungano huo David Kiplimo ameshinikiza kuhamishwa kwa Maafisa hao wa Trafiki kutokana na kukaa kwao katika kituo cha Kapsabet kwa muda mrefu.
Hata hivyo wakuu wa chama hicho waliipongeza Kaunti ya Uasin Gishu kwa huduma bora wanazotoa katika sekta ya usafiri huku wakiishtumu Kaunti ya Nandi kwa huduma mbaya.