Wahudumu wa pikipiki katika mtaa wa Katisha huko Kisauni wamekashifu vikali hatua ya kuhangaishwa kwa baadhi ya wakazi na vijana wadogo waliokuwa wamebeba rugu usiku wa kuamkia leo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Vijana hao waliotokea sehemu za Barsheba waliwatia wasiwasi wenyeji baada ya kupitia vichochoroni kwa kuchukua nafasi ya barabara nzima kwa kuwafurusha wahudumu wa bodaboda waliokuwa wakiendelea na shuhuli zao za kila siku katika kituo cha Mgongeni na Katisha Mtawalia.

Kulingana na Jacob Mtawali, Mkazi wa mtaa wa Katisha, anasema alikutana na vijana hao ana kwa ana alipokuwa akielekea dukani na wakamzingira alipokuwa akijaribu kuwakwepa.

Mtawali ambaye aliwahusisha vijana hao na kundi la wakali kwanza, anasema vijana hao walipitia barabara ya Mgongeni kuelekea Kisimani mara tatu kabla ya mzee wa mtaa wa eneo hilo kupiga ripoti kwa maafisa wa polisi katika kituo cha polisi cha Nyali.

Anasema vijana hao walikuwa takribani kumi walikuwa wamejihami sio tu kwa rungu bali pia walikuwa na visu huku akiongeza kuwa haijulikani vizuri kama walikuwa na silaha zaidi kwani walikuwa wamebeba mabegi anayosema anaamini yalikuwa na sila nyengine.

Aidha kwa upande wake Joel Kaki mhudumu wa bodaboda anayeegesha kwenye kituo cha Katisha, vijana hao walikuwa wakali mno kwani waliwapiga kwa rungu wahudumu wa pikipiki waliokuwa barabarani na wakiwasafirisha wateja wao.

Kwa sasa wameitaka serikali kuu pamoja na ile ya kaunti ya Mombasa kujenga kituo cha polisi katika eneo hilo ili kudhibiti visa vya mara kwa mara vya utovu wa usalama.

Kisauni ni mojawapo ya mitaa hapa mjini Mombasa inayokumbwa na utepetevu wa usalama kwa kikubwa huku ukihusishwa pakubwa kuwa makazi ya genge la wakali kwanza.