Wahudumu wa pikipiki mjini Molo wameamua kuweka matuta katika barabara muhimu mjini humo, baada ya ongezeko la ajali kushuhudiwa ambapo watu kadhaa wamepoteza maisha yao katika siku za hivi majuzi.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Madereva hao wamesema wameafikia hatua hiyo, baada ya kilio chao kupuuzwa na mamlaka ya kitaifa ya usimamizi wa barabara KeNHA, pamoja na bodi ya kitaifa ya kusimamia usalama barabarani (NTS).

Wakiongozwa na katibu wa kundi la wahudumu wa bodaboda wilayani humo John Kagwa, madereva hao wa pikipiki wamesema wamepelekea mamlaka hizo malalamishi, lakini hadi sasa lalama zao hazijatiliwa maanani.

Wamesema baada ya barabara mjini humo kuwekwa lami mwazoni mwa mwaka jana, ongezeko la ajali limeshuhudiwa baada ya wanakandarasi kukamilisha miradi ya ukarabati wa barabara bila kuweka matuta.

Kagwa amesema muungano wa wahudumu wa pikipiki ulifanikiwa kugharamia vifaa vya ujenzi wa vidhibiti kasi hivyo, pamoja na kusimamia wataalam wakuweka matuta hayo kama hatua moja ya kupunguza ajali mjini Molo.

“Badala ya barabara hii kuwa baraka kwetu, kila siku kumekuwa na visa vya ajali. Watu wengi wamepoteza maisha yao huku wengine wakilemaa baada ya kuhusika kwenye ajali. Leo tumechukua hatua ya kuweka matuta kwa lengo la  kupunguza ajali,” alisema Kagwa.