Wahudumu wa tuktuk katika eneo la Buxton mjini Mombasa wamelalamikia kuhangaishwa mara kwa mara na maafisa wa trafiki.
Wakiongea na mwandishi huyu katika kituo cha magari cha Buxton siku ya Jumanne, wahudumu hao walisema kuwa kwa sasa imekuwa kama desturi kwa baadhi ya maafisa wa trafiki kutoka kwa serikali kuu na wale wa serikali ya Kaunti ya Mombasa kuwasimamisha kila wanapoendesha shughuli zao.
Wahudumu hao walisema kuwa kila wanaposimamishwa na maafisa hao, wengi wao huishia kuwaitisha rushwa haswa wale ambao hawana stakabadhi za kuhudumu katikakati mwa mji.
Hussein Omar, mhudumu wa tuktuk alisema kuwa amekamatwa mara kadhaa na maafisa wa polisi kwa kisingizio eti hana stakabadhi za kuhudumu katikati mwa mji.
Alisema kuwa hatua hiyo ni kinaya kikubwa kwani hata anapowatolea na kuwaonyesha maafisa hao stakabadhi hizo, wao huishia kutafuta kosa lingine almradi waweze kupata pesa kutoka kwake.
Alisema kuwa maafisa wanaohudumu wakati wa usiku haswa siku ya Ijumaa ndio waliona na tabia hiyo.
Kwa upande wake, Daniel Chiro alisema kuwa hatua ya ulaji rushwa miongoni mwa maafisa wa trafiki ndio ambayo imepelekea ongezeko la ajali zinazohusisha tuktuk mjini Mombasa.
Alisema kuwa kwa sasa serikali inapaswa kubuni njia mwafaka za kushughulikia tatizo hilo.
Aidha, amewataka wakuu wa trafiki kuingilia kati jinsi maafisa wao wanavyoendesha shughuli zao akisema kuwa wengi wa wahudumu wamechoshwa na tabia za ulaji hongo.