Wahudumu wa tuktuk katika eneo la Kisiwa cha Mombasa na Likoni wamelalamikia ukosefu wa abiria hususan wale ambao hutumia kivuko cha feri cha Likoni, kwa kile walichokitaja kama nauli ya juu.
Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatatu katika kituo cha kuegesha tuktuk cha Buxton, wahudumu hao wakiongoza na Alfred Owino, walisema kuwa abiria ambao huabiri tuktuk wakitaka kuvukishwa hadi ng’ambo nyengine, hulalamika kuwa nauli wanayotozwa ni ya bei ya juu.
Wahudumu hao walisema kuwa wao hulazimika kuwalipisha abiria hao nauli hiyo ya kiasi cha juu kwa sababu huwa kuna malipo ambayo wanatakikana walipe kwa Shirika la Huduma la Feri KFS.
Owino aliitaka shirika hilo la KFS kushughulikia swala hilo na kupunguza ada ambayo wahudumu hao hutozwa ili kuleta afueni kwa abiria.
Aidha, alisema kuwa hali hiyo ikiendelea kuwa hivyo basi, watalazimika kufanya kazi bila kupata hata akiba ya kuweka ili kujisaidia baadae.
“Naweza kaa hapa maskani kwa muda wa masaa matatu bila kupata hata shilingi moja kwa sababu wateja wengi ambao huwa na mizigo hutaka kuvukishwa hadi ng’ambo ya pili kuenda Likoni. Hatahivyo, nikiwaambia bei yangu huwa wanakataa na mimi siwezi fanya kazi ya hasara,” alisema Owino.
Wahudumu hao wameomba usaidizi kutoka kwa serikali ya kitaifa pamoja na ile ya kaunti, ili waweze kupata afueni.
Kwa upande wake, Shirika la huduma la Feri KFS, imesema kuwa ada hiyo inayotozawa si ya juu ila ndio kiwango cha kawaida.