Katibu wa chama cha wahudumu wa tuktuk cha Mokotuo Sacco, John Kinyanjui, amesema kuwa watashirikiana na idara ya trafiki kuwatambua madereva wanaomiliki vibali bandia.
Akizungumza kwenye hafla ya kutoa leseni kwa wanachama wa muungano huo, Kinyanjui alisema kuwa vijana wengi wamekuwa na desturi ya kupiga chapa leseni za wenzao na hata kuunda leseni bandia ili waweze kuhudumu kama madereva.
Alisema kuwa hatua hiyo imekuwa ikiharibia muungano huo jina.
“Wahudumu wa tuktuk wanapokamatwa na vibali hivyo bandia, wao huwaambia maafisa wa trafiki kuwa sisi ndio tuliowapa leseni hivyo,” alisema Kinyanjui.
Kinyanjui alisema kwamba ni jambo la kusikitisha kuona kwamba idadi ya wanaotiwa nguvuni kutokana na udanganyifu wa leseni inaendelea kuongezeka, huku kila wanapokamatwa wanaolaumiwa wakiwa maafisa wa muungano.
Aliahidi kuungana na idara ya trafiki kudhibiti ajali zinazochangiwa na kutojua alama za barabarani.