Wahudumu wa tuktuk katika mitaa inayokumbwa na utovu wa usalama wametakiwa kutojihusisha na makundi hasimu yanayoendeleza uovu mjini Mombasa.
Haya yanajiri baada ya tuktuk mmoja kupatikana ikiwasafirisha vijana waliokuwa wamewaibia wenyeji katika mtaa wa Katisha huko Kisauni.
Akizungumza baada ya kupata ripoti kutoka kwa wakaazi wa eneo hilo, mkuu wa polisi katika eneo la Kisauni Richard Ngatia alisema kuwa kwa sasa imekuwa kama desturi kwa wahudumu wa tuktuk kuwasafirisha wezi pindi tu wanapotibuliwa na wenyeji.
“Vijana hao ambao huwa mara nyingi wamenusurika husafirishwa na tuktuk na kukimbilia mjini ambako wanaaminika kwenda kujificha kwa marafiki wao. Huenda wahudumu hao wakawa ndio wanaowaelekeza vijana mahali pa kuiba kwani hali hiyo imekuwa ikishuhudiwamara nyingi mtaani humo,” alisema Ngatia.
Akitoa mfano wa hivi majuzi ambapo tuktuk ilionekana ikiwasafirisha takribani vijana watano kutoka mtaa wa Kisauni na kuwashukisha eneo la kituo cha magari cha Buxton, Ngatia alisema vijana hao walikuwa wameshatekeleza maovu mtaani Katisha na hiyo ilikuwa njama ya kuwakimbiza ili waepukane na adhabu iliyowajaa wakaazi.
Aidha, kulingana na Mzee Jacob, aliyeshuhudia kisa hicho, vijana hao waliwapora wahudumu wa duka la Mpesa mtaani humo na kutorokea eneo la Frere Town.
Jacob ameitaka idara ya usalama kutilia mkazo swala la usalama eneo hilo kwa kuwachunguza wahudumu wa tuktuk pamoja na wale wa pikipiki.