Waziri wa ugatuzi Ann Waiguru amewapa changamoto vijana na kina mama katika kaunti ya Kisii kuchukua nafasi iliyoko kuomba pesa ambazo wametengewa na serikali.
Waiguru, ambaye ni waziri wa Ugatuzi alikuwa akiongea katika kaunti ya Kisii, kwenye ukumbi wa Cultural siku ya Jumatatu alipokuwa kwenye ziara ya kuyapokeza makundi mbalimbali pesa za Uwezo Fund na zile za vijana na za kina mama kwenye kaunti ya Kisii.
Kundi la kina mama la Mosweta liliweza kupokea pesa nyingi zaidi miongoni mwa makundi ya kina mama, ambapo walipokea elfu mia tatu hamsini, na kwa upande wa vijana kundi la Makutano lilipokezwa hundi ya shilingi elfu 100.
Waziri huyo alisema kuwa serikali pia imewapa vijana na kina mama kapau mbele katika masuala ya kandarasi za serikali, ambapo wametenga asilimia 30 kwa makundi hayo na akawaomba vijana nakinamama ambao walikuwa ukumbini kuandika mapendekezo kwa serikali ili kuuza kandarasi zao na iwe njia mojawapo ya kujienmdeleza kimaisha.
Kaunti ya Kisii ilipokezwa shilingi milioni 7.9 kwa jumla ya pesa zote. Hundi nyingine ya shilingi milioni 5.7 kwa vijana kwa jumla ya kiwango hicho kilichopokezwa kaunti.
"Nawaomba vijana na kina mama ambao mko hapa muwe mnaomba mikopo hii ambayo serikali imewatengea..Uwezo fund iko, pesa za vijana na kina mama zote ziko kwa ajili yenu" alisema Wiguru.
Naye Gavana James Ongwae alimshukuru Waiguru kwa juhudi zake za kuendeleza masuala ya ugatuzi, na pia kuhakikisha kuwa vijana na kina mama wanaangaziwa zaidi wakiwa ndio wengi katika nchi yetu.
“Asante sana Bi Waiguru kwa kutembelea kaunti yetu na kujali kina mama na vijana wetu ambao ni wenye bidii sana katika biashara na ukulima na hii pesa itawafaa kwenye biashara zao,” alisema Ongwae.
Bi Waiguru aliandamana na viongozi kutoka Kisii akiwemo gavana Ongwae, seneta Mogere Obure, Momoima Onyonga, Jimmy Nuru, Zebedeo Opore, Onyancha Joel miongoni mwa viongozi wengine kutoka kaunti ya Kisii.